Judegment Day At The High Court London

Judegment Day At The High Court London
Mengi v Hermitage: Libel Claim Successfully Defended

Saturday 12 May 2012

Ya Hosea nayo ni ‘simply beyond satire’ ?

 

Home

 

Johnson Mbwambo

Toleo la 236

25 Apr 2012

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah, kwa mara nyingine, huko Dodoma, amewasilisha ripoti ya mwaka inayochefua.

Hata hivyo, safari hii mambo yalikuwa tofauti. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa, ripoti yake ya ukaguzi iliwasha moto mkubwa bungeni Dodoma ambao nusura uwaangamize mawaziri wanane wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Tofauti na ilivyokuwa kwenye ripoti zake za nyuma alizoziwasilisha bungeni, safari hii baada ya Utoah kuwasilisha ripoti yake inayoonyesha namna ufisadi mkubwa unavyoendelea kutafuna fedha za walipakodi, wabunge walichachamaa na kuwataka wabunge wanane wanaotuhumiwa kwa ufisadi waachie ngazi.

Kilichotokea huko Dodoma, wiki iliyopita, kinaweza sasa kuwa ni historia, lakini, kwa mtazamo wangu, ni wakati mwafaka wa kutathmini utendaji wa Edward Hosea na asasi yake (TAKUKURU) iliyopewa dhamana ya kuendesha vita dhidi ya ufisadi nchini.

Kwa hiyo, tafakuri ya leo tumtathmini Edward Hosea na TAKUKURU yake. Hata hivyo, kwangu ni kitu kigumu kumtathmini mtu ambaye ulikutananaye kwa mara ya mwisho zaidi ya miaka 30 iliyopita, na ndiyo sababu nafanya hili kwa uangalifu mkubwa.

Nilimfahamu Edward Hosea miaka ile miwili ya 1976 na 1977 wakati tukisoma wote kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Mzumbe, Morogoro, tukikaa wote bweni moja liitwalo Milambo.

Namkumbuka alikuwa kijana mchapakazi (darasani), muungwana, mtanashati na mmoja wa waliokuwa wakiongoza kwa usafi wa sare zao za shule pale Mzumbe.

Miaka yote miwili pale Mzumbe sikupata kumwona Edward Hosea akiadhibiwa kwa kosa lolote au akiwa amevaa sare zilizochafuka au viatu ambavyo havijui kiwi kwa mwezi mzima; tofauti na ilivyokuwa kwa sisi wengine!

Tangu tuondoke pale Mzumbe, sijapata kukutana na Edward Hosea hata mara moja; japo nimekuwa nikifuatilia kwa karibu maendeleo yake kitaaluma, kupitia vyombo vya habari, hadi alipoteuliwa kuwa bosi mkuu wa asasi ya kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU).

Kwa kigezo cha uungwana wake na uchapakazi wake nilioushuhudia tulipokuwa pale Mzumbe miaka karibu 35 iliyopita, imekuwa vigumu kwangu kuyaamini haraka yale ‘madongo’ anayorushiwa kuhusu utendaji wake tangu awe bosi mkuu wa asasi hiyo ya kupambana na ufisadi nchini.

Lakini kiasi miaka inavyosonga mbele, huku ikidhihirika kuwa TAKUKURU imewashindwa mapapa wa ufisadi nchini, ndivyo pia ninavyozidi kuamini uhalali wa ‘madongo’ hayo kwamba vita dhidi ya mafisadi papa imekuwa kubwa mno kwake kuipigana.

Na ushahidi u-dhahiri. Tangu ateuliwe kuwa bosi mkuu wa asasi hiyo, ni fisadi gani papa ambaye leo yuko jela kwa sababu ya kazi nzuri ya Hosea na TAKUKURU yake? Kama yupo, nitajieni.

Na nazungumzia mafisadi papa na si hawa vidagaa wa mikoani (hakimu, polisi, mwalimu, katibu kata nk) kwa sababu moja kubwa; nayo ni kwamba fisadi mmoja papa huweza kukomba mabilioni ya pesa za walipakodi kwa dili moja tu. Na kama hivyo ndivyo, wakiwa kumi si wanaweza kabisa kuifilisi serikali?

Hata hivyo, nashindwa kuelewa ni nini kinachomfanya Edward Hosea aishindwe vita hii dhidi ya mafisadi papa? Ni kwa sababu ya kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa aliyemteua – Rais Kikwete au ni kukosa tu yeye binafsi dhamira ya kutosha kupambana na uovu huo?

Mwaka juzi (2010) mtandao ule wa Wikileaks uliwahi kuvujisha habari kuwa Edward Hosea aliwahi kumwambia balozi wa Marekani hapa nchini kwamba Rais Kikwete ndiye aliyemzuia kuwafikisha mahakamani baadhi ya mafisadi papa nchini.

Kwa kuwa asilimia 90 ya habari zilizovujishwa na Wikileaks zilikuja kuthibitishwa baadaye kuwa ni za kweli, sina sababu ya msingi ya kutoamini kuwa Hosea hakumwambia hivyo mwanadiplomasia huyo wa Marekani; licha ya yeye mwenyewe kukanusha - pengine akihofia hasira za Kikwete dhidi yake.

Lakini kama ni kweli kuwa kushindwa kwake kupambana na mafisadi papa kunatokana na kufungwa ‘gavana’ na Rais Kikwete, ni kwa nini basi school mate wangu huyu haulindi uungwana wake ule wa zama za Mzumbe kwa kujiuzulu ubosi wa TAKUKURU?

Wiki iliyopita, huko Dodoma, wabunge walicharuka kuhusu kiwango cha ufisadi serikalini na katika mashirika ya umma hadi kufikia hata hatua ya kutaka mawaziri kadhaa wafukuzwe.

Na si hivyo tu, walifikia hata hatua ya kujaribu kumpigia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kura ya kutokuwa na imani naye kwa kushindwa kuwadhibiti mawaziri hao mafisadi.

Msingi wa hasira za wabunge na wananchi kwa ujumla ni ripoti za kila mwaka za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo kila mwaka zinaonyesha ufisadi wa kutisha; huku kukiwa hakuna hatua zozote kubwa za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Kwa hakika, kwa hilo, TAKUKURU nayo haiwezi kukwepa hasira za wabunge na hasira zetu sote juu ya jambo hili. Ukiuchunguza ushahidi wa ufisadi wa baadhi ya mawaziri unaoanikwa na kamati za bunge; achilia mbali ule unaoanikwa mara kwa mara na vyombo vya habari (likiwemo gazeti hili), ni vigumu kuamini kama kuna chombo hapa nchini kinaitwa TAKUKURU kinachofanya kazi yake ipaswavyo!

Kwa maneno mengine, ripoti za kila mwaka za CAG, ushahidi wa wabunge kuhusu ufisadi wa baadhi ya mawaziri na skandali za kifisadi zinazoanikwa magazetini mara kwa mara, ni ushahidi wa kutosha kwamba TAKUKURU imeshindwa kazi.

Maana, kama asasi hiyo ingekuwa haijashindwa kazi, ingekuja na ripoti yake yenye ushahidi wa idadi ya mawaziri au vigogo wowote iliowafikisha mahakamani kwa ufisadi kwa kiopindi hata cha miaka miwili tu iliyopita.

Nijuavyo, kama TAKUKURU ina orodha ya namna hiyo, basi, itakuwa imejaa majina ya vi-fisadi dagaa; yaani karani hapa, polisi pale, hakimu wa mahakama ya mwanzo kule....nk!

Ni kwa kuzingatia yote hayo ushauri wangu kwa school mate wangu Hosea ni huu: “Achape kazi, akamate mafisadi papa na kuwafikisha mahakamani, na endapo anayemkwamisha kufanya hivyo ni Rais, basi, aonyeshe uungwana kwa kujiuzulu ili alinde heshima yake.

Vinginevyo, school mate wangu huyu ataendelea kurushiwa ‘madongo’ ya utendaji hovyo wa TAKUKURU. Na kwa hakika, unapozungumzia ‘madongo’ dhidi yake, nalikumbuka hili lililowekwa majuzi kwenye mtandao wa African Arguments.

Katika ‘dongo’ hilo, mwanasheria wa Uingereza na mwanaharakati wa vita dhidi ya ufisadi, Sarah Hermitage, anamponda Hosea kwa kauli yake aliyoitoa kwenye gazeti la Daily News, Machi 31, 2012, kwamba eti hakuna Mtanzania aliyehusika kwenye kashfa ile ya rada!

Sarah Hermitage anaandika kwa uchungu kabisa akikemea kauli hiyo ya Hosea kuwa si ya kiuwajibikaji, na anashangaa ni kwa nini serikali yake (ya Uingereza) haijatoa taarifa rasmi kuhusu kauli hiyo.

Sarah Hermitage alifikia hatua ya kumwita Hosea kuwa ni msanii, na kwamba kauli yake hiyo kuwa hakuna Mtanzania aliyehusika na ufisadi huo wa rada ni “simply beyond satire”; yaani ni ya kupita usanii wa kawaida tuliouzoea!

Katika hilo, hata mimi naungana na Sarah Hermitage, na naamini Watanzania wengi pia wanaungana naye. Yaani; Hosea anataka kutuaminisha kuwa katika kashfa ya rada hakuna hata Mtanzania mmoja aliyehusika? Yaani, waliohusika si Andrew Chenge wala si Shailish Pragji Vithlan; bali ni Waingereza wenyewe?

Si imesemwa it takes two to tango. Sasa, kama kwa upande wa Waingereza waliohusika ni BAE Systems, kwa Tanzania ni nani? Hosea atujibu hili.

Anasema kwa Tanzania hakuna fisadi papa aliyehusika? Je Watanzania tumwamini Hosea? Jamani, si Hosea huyu huyu ambaye mwaka jana alitupiana maneno na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi, kuhusu ‘lilikopotelea’ faili la Chenge la kashfa ya rada?

Wasiolikumbuka vyema tukio hilo ni kwamba, Hoseah alikuwa ameliwasilisha faili hilo kwa DPP baada ya kukamilisha uchunguzi wake, na dhahiri alitaka kibali cha kufungua mashitaka, lakini Feleshi akawaambia waandishi kuwa hajapelekewa faili hilo, na wawili hao wakaendelea kulumbana kidogo magazetini kuhusu faili hilo.

Sasa leo inakuaje Hosea huyo huyo aseme hakuna Mtanzania aliyehusika kwenye kashfa ya rada? Je, tumwamini?

Sarah Hermitage anasema kauli hiyo ya Hoseah ni simply beyond satire – ni usanii uliopitiliza; nami nakubaliana naye kwa asilimia 100.

Nihitimishe kwa kukumbusha kwamba wahisani wa nje wameanza kuishiwa na uvumilivu kwa jinsi watawala wetu wanavyowalinda mafisadi papa nchini.

Majuzi tu hapa, akiandika kwenye gazeti maarufu la Uingereza la Financial Times, Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Kenya, Sir Edward Clay, alisema kuwa ile kansa iliyokuwa ikiitafuna Kenya ya kuwalinda mafisadi, imehamia Tanzania.

Huyu ndiye yule balozi aliyepata kuwakejeli watawala wa Kenya kuwa: “Wanatafuna fedha za umma kwa ulafi, na kisha wanakwenda kutapika kwa shibe kwenye miguu ya wahisani”. Nionavyo, muda si mrefu watawala wetu nao wataangukia kundi hilo.

Vyovyote vile; nihitimishe kwa kuwapongeza wabunge wote wa CCM walioweka tofauti zao za kichama pembeni na kuungana na wenzao wa CHADEMA kuichachafya Serikali huko Dodoma kwa kulea ufisadi. Laiti tungekuwa na rais msikivu....!

Tafakari.

No comments: